Wavuvi wakishusha samaki baada ya kuwavua
katika Ziwa Victoria. Uvuvi haramu umesababisha
kitoweo hicho kuwa adimu sana kwenye ziwa hilo.
katika Ziwa Victoria. Uvuvi haramu umesababisha
kitoweo hicho kuwa adimu sana kwenye ziwa hilo.
MAJUZI, niliambiwa na ndugu zangu fulani wanaoishi huko kanda ya Ziwa kwamba walikaribia kumzika binamu yangu mmoja ambaye inahofiwa kwamba alikula samaki aliyevuliwa kwa sumu kali ya Thiodan.
Ingawa inaonekana kwamba binamu yangu huyo hakuwahi kupimwa hospitalini ili daktari kuthibitisha kwamba iliyokuwa inamsumbua ni sumu, lakini nilipata maelezo ya kutosha kwa nini kuna hisia hizo. Aidha hii pia inaonesha adha ya maisha ya vijijini ambako hakuna madaktari (isipokuwa waganga wasaidizi vijijini) na hospitali zisizo na vipimo.
Kinachoonesha kwamba binamu yangu huyo alikaribia kupoteza maisha kutokana na kula samaki aliyevuliwa kwa sumu ni ukweli kwamba hata watu wengine waliokula mlo huo walikumbwa na tatizo la tumbo. Kingine ni baada ya kugundulika kwamba sehemu fulani ya ziwa hilo walikutwa samaki wakielekea, hali inayoonesha kwamba kuna washenzi walimwaga sumu eneo hilo.
Ndio, ni washenzi na ndilo jina linalowastahili na mimi sioni kosa hata idogo kuwaita hivyo! Cha mwisho, ni maelezo niliyoyapata kwamba baadhi ya wanakijiji waliwashitukia wachuuzi waliokuwa na samaki hao kwamba wana mushkeli baada ya kuwaona wakiwa wanatoa ute kwenye matumbo yao huku pia matamvua yao yakiwa yamebadilika.
Ndio, ni washenzi na ndilo jina linalowastahili na mimi sioni kosa hata idogo kuwaita hivyo! Cha mwisho, ni maelezo niliyoyapata kwamba baadhi ya wanakijiji waliwashitukia wachuuzi waliokuwa na samaki hao kwamba wana mushkeli baada ya kuwaona wakiwa wanatoa ute kwenye matumbo yao huku pia matamvua yao yakiwa yamebadilika.
Hili lilinikumbusha sentensi hii niliyowahi kuambiwa na mwanakijiji mmoja, Lumumba Chisumo, nilipotembelea kijiji kiitwacho Mugango, mwaka jana: “Wanavizia usiku, kisha wanamwaga sumu katika eneo la kama heka moja tu. Kwa muda mfupi tu wanazoa hadi tani 50 za samaki na kukimbia na maboti yao. Kwa kweli ni hatari sana."
Lumumba akazidi kuniambia: “Siku ya pili yake, unakuta samaki kibao wakiwa wameelea hovyo ziwani na kutapakaa kila mahala. Kwa kweli, licha ya kutishia sana maisha ya walaji, hawa jamaa (washenzi) wanatishia sana uhai wa viumbe hawa wa ziwani ambao tumekuwa tukiwategemea miaka nenda miaka rudi”.
Niliambiwa pia kwamba wavuvi hawa haramu huwa hawachukui samaki aliyekufa katika eneo la tukio, na hivyo huchukua tu wale waliolewalewa, ambao kimsingi huwa hawana sumu hadi kwenye matumbo yao.
“Wanaacha waliokufa na ndio maana samaki hujazana ziwani kiasi kwamba baada ya siku mbili ukipita ziwani samaki wananuka kila sehemu. Wale wanaowachukua huwa hawana sumu sana na hawaozi. Unajua samaki walioshiba sumu sawasawa huoza haraka na hawawezi hata kuwafikisha kwenye soko,” akaniambia Lumumba.
Mwanakijiji mwingine, Zida Mayogu, aliniambia hivi: “Siku moja tuliona boti mpya kabisa ziwani, tukawa tunadhani ni maofisa maliasili. Wengine wakawa wanadhani ni watu tu wa kawaida, asubuhi yake kulipokucha tukakuta samaki wameleea kibao ziwani. Tukajua kumbe walikuwa wavuvi wa sumu.”
Akasema kwamba kuna wakati wavuvi hao wanakuja usiku usiku na kutia nanga majini wakivizia usiku ufike, kisha wanamwaga sumu na kuzoa samaki kabla ya kuondoka.
Wanakijiji waliniambia kwamba wavuvi wa sumu mara nyingi huwa na silaha za kisasa, hususan bunduki, na ndio maana wanakijiji huogopa kuwasogelea hata wakihisi kwamba wapo sehemu fulani.
Nilichogundua katika kuwahoji watu mbalimbali kuhusu tatizo hilo ni kwamba wavuvi wa kawaida, yaani wananchi wa maeneo ya mwambao wa Ziwa Victoria, hawapendi kabisa uvuvi huo na wanauchukia sana.
Kitu ambacho mpaka leo bado ninajiuliza ni hiki: Kwa nini uvuvi huu haramu umeendelea kuwepo na ni nani hasa wanaojihusisha na uvuvi huu?
Ingawa utafiti zaidi unaweza kufanywa ili kugundua hilo, lakini kutokana na majibu ya watu mbalimbali niliopata kuwahoji mwaka jana ni kwamba uvuvi huu unaendelea kushamiri kwa sababu wahusika wake wanakingiwa kifua na wakubwa, wakiwemo viongozi wa vijiji, maliasili na hata polisi!
Inaelezwa kwamba siku wageni hao hatari wanapozuru maeneo wanayotaka kufanya uhalifu, viongozi wa vijiji, wakiwemo maofisa maliasili huwa hawaonekani.
“Si rahisi wakafanya uvuvi huu bila kushirikiana na wakubwa fulani fulani wakiwemo maofisa wa juu kabisa wa polisi,” aliniambia Muneji Mayogu, binti anayeishi katika kijiji cha Kurwaki, Mugango.
Mtu mwingine niliyeongea naye mjini Musoma kwa sharti la kutotajwa jina lake, aliniambia kwamba yeye anao ushahidi wa karibu asilimia 100 kwamba baadhi ya mabosi wa polisi ama wake zao na ndugu zao, ndio hodari katika kuendesha uvuvi huo haramu.
Kwa vile wavuvi hawa hatari hukusanya kiasi kikubwa cha samaki, hususan sato (kwa vile sato wana tabia ya kukaa juu juu ya maji), pia wana pesa nyingi tu na kwa vile jamii yetu imeoza kwa rushwa na ufisadi, inaonekana itakuwa vigumu sana kuuondosha uvuvi huu hatari kwa maisha ya watu na maliasili zingine zilizoko ziwani.
Kumbukumbu zangu zinaonesha kwamba iliwahi kufanyika semina moja mjini Bukoba, ambapo mtoa mada mmoja alisema kwamba wavuvi wa sumu, wakionekana wapigwe kama wachawi!
Hii ilikuwa ni sawa na kuwahamasisha wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa kuwapiga, na hata kuwaua wavuvi wa sumu. Na bila shaka matamshi ya mtoa mada huyo ambaye ni ofisa wa serikali, yangeweza kumtia misukosuko mingi.
Lakini kikubwa cha kujiuliza ni kwa nini mtu akafikiria kuhamasisha wananchi kumchukulia mvuvi wa sumu kama mchawi na kushauri apigwe, na inaonekana wananchi waliokuwa kwenye semina walishangilia!
Ni habari ya matukio ya wavuvi wa aina hii wanakamatwa kupigwa na wananchi mpaka kuuliwa. Bila shaka ni kwamba wananchi wamechoka na huenda hawaoni kama sheria inafuatwa sawasawa kwa wanaokamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Hata wakati nilipokuwa ninaongea na wavuvi kule kijijini walinijibu vivyo hivyo kwamba wao wakimfuma mvuvi haramu ama mwizi wa nyavu za kuvulia samaki ni kuua tu na hakuna cha mjadala.
Kuna wakati Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwafananisha wavuvi wanaotumia sumu ama hata mabomu kwamba ni wauaji. Kwa msingi huo, Mwalimu Nyerere alikuwa anawaona watu hawa wanaostahili kuhukumiwa kifo kama watapatikana na hatia.
Hata mimi, na hii ni mara ya tatu kuandika makala kuhusu uvuvi wa kutumia sumu, ninaungana na Mwalimu Nyerere kuwaona wavuvi hawa kwamba ni wauaji kwa sababu wanahatarisha maisha ya walaji. Licha ya hivyo, wanasababisha madhara katika uchumi kwani kuna wakati walisababisha samaki wetu wakafungiwa kuingia katika soko la Ulaya.
Mimi kwa vile si mwanasheria, kwa kweli sijui mvuvi wa sumu anapokamatwa na kufikishwa mahamani na kisha kupatikana na hatia anapewa adhabu gani?
Ninahisi adhabu iliyopo ni ndogo sana kulinganisha na madhara anayoyaleta mvuvi wa aina hii kwa kuweza kusababisha kifo na kuua samaki wengi pamoja na mayai.
Ndio maana nimekuwa mara kwa mara nikiomba taasisi zinazohusika na mambo ya maliasili, 'kulobi' kwa wabunge wafikirie sasa kutunga sheria kali dhidi ya wadhalimu kama hawa, pengine ikasaidia kuwahofisha watu kushiriki katika ufisadi huu.
Ninajua kwamba kuna makosa makubwa kama ya kuua, kuhujumu uchumi, kubaka na uhaini. Kama uvuvi haramu wa samaki haujajumuisha katika makosa makubwa kama haya, basi wahusika wafanye haraka sana ikiwezekana.
Sambamba na sheria, lazima mambo kama askari kulinda maliasili hii kwa kutumia boti zinazokwenda haraka inaweza kusaidia sana, ingawa kwa vile jamii yetu imeoza kwa rushwa, huu unaweza kuwa tena mradi wa hao watakaopewa maboti na pengine wao ndio wakawa tena wavuvi wakubwa wa sumu!
Na kwa vile baadhi ya vigogo wa serikali na polisi wanadaiwa kujihusisha na biashara hii haramu, pengine ni wakati mwafaka kwa serikali kuwahamisha hamisha na kuwapeleka katika maeneo mengine yasiyo na ziwa, huenda wakaja vigogo wengine ambao watanusuru maliasili hizi.
Kwa vile jamii yetu karibu yote inaugua kansa ya rushwa, ndio maana nashauri askari na maofisa wa maliasili kuhamishwa hamishwa. Na pia ninaona umuhimu wa Rais kuunda tume ya kuchunguza tatizo hili, hususan kanda ya ziwa, na kutoa ushauri wa kitalaamu wa namna litakavyoondoshwa.
No comments:
Post a Comment