WAKATI wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Mbunge wa Jimbo la Masasi (CCM), Mariam Ruben Kasembe, alizishambulia tafiti mbalimbali zinazofanywa nchini na taasisi kama HakiElimu na kisha kutangazwa kwenye vyombo vya habari kuwa hazina maana yoyote zaidi ya kuidhalilisha serikali.
Mbunge huyo alidai kwamba wananchi hawayapendi matangazo ya HakiElimu, na hivyo akashauri eti ni heri pesa zinazotumika kwenye tafiti, machapisho na matangazo hayo zipelekwe kwenye maeneo husika yenye matatizo.
Mawazo ya mbunge huyu wa CCM hayana tofauti na yale ya wabunge wawili wa chama hicho ambao mwaka 2007 waliitaka serikali kuichukulia hatua HakiElimu kwa maelezo kuwa matangazo yake yamekuwa yakibeza juhudi za kuendeleza elimu nchini zinazofanywa na serikali.
Wabunge walioonekana kukerwa na HakiElimu wakati wakichangia bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (2007), walikuwa Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa ambaye pia kwa sasa ni Naibu Spika na Janet Masaburi (Viti Maalumu).
Wakati Ndugai alidai kuwa matangazo hayo yanaweza kuiangusha serikali, Masaburi, alidai yanajenga chuki miongoni mwa wananchi dhidi ya serikali yao.
Ikumbukwe pia kwamba serikali iliwahi kupiga marufuku matangazo ya asasi hiyo isiyo ya kiserikali na watu wengi walijitokeza kuitetea HakiElimu wakiishaanga serikali kwa hatua hiyo. Baadaye Serikali iliifungulia taasisi hiyo kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Balozi Mwapachu |
Tumeshindwa kujua kile ambacho kimekuwa kikiwakera wabunge wa CCM na hata serikali kuhusu ukweli unaowekwa wazi kwa njia ya machapisho na matangazo na taasisi ya HakiElimu na zingine za aina hiyo, kama Uwezo ambayo mapema mwaka huu ilitoa taarifa ya utafiti wake unaoonesha kuwa nchi yetu iko nyuma kielimu kulinganisha na wenzetu wa Kenya na Uganda.
Tunachojua sisi, machapisho ama matangazo yanayotolewa kwa njia ya maigizo na taasisi hizi hayaji kwa kukurupuka bali yanatokana na tafiti. Kwa lugha nyingine, tafiti hizi tunazooneshwa kwa njia ya matangazo na machapisho zinalenga kutufumbua macho na kutuzindua kama taifa kuhusu hali halisi ilivyo ili tuchukue hatua na hivyo wahusika walitakiwa kupongezwa na si kubezwa, kutishwa ama kufungiwa.
Tunaandika haya tukijua kwamba nchi yetu bado ina kiwango kidogo sana cha tafiti na kwamba hatuwezi kuweka mipango yoyote ya maana ya maendeleo bila kusaidiwa na tafiti.
Tunajua kwamba serikali imekuwa ikijitahidi kufanya maendeleo katika elimu lakini hiyo haimaanishi kwamba mambo kila siku yako shwari isipokuwa tafiti hizi ndizo zinatakiwa kuizindua serikali na jamii kwa ujumla ili kujua namna nzuri ya kutumia raslimali chache zilizopo kwa ajili ya maendeleo yetu.
Na tumeshindwa kujua kwa nini Mbunge Kasembe anawasingizia wananchi kwamba matangazo ya HakiElimu yanawaudhi, jambo ambalo tunaamini hajalifanyia utafiti. Matangazo ya HakiElimu yanaamsha hisia chanya kwa wananchi ili kuwawajibisha viongozi wao kuhusu cha kufanya kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya watoto wao.
Wakati akizindua taarifa ya taasisi ya Uwezo kuhusu utafiti wao mapema mwaka huu, Balozi Juma Mwapachu alisema kwamba tafiti hizi zinalenga kuangalia kwa kina matatizo yanayoikabili sekta ya elimu katika nchi yetu na namna ya kuyapatia ufumbuzi kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu.
Balozi Mwapachu alikaririwa akisema: “Ifike wakati tuzitumie tafiti hizi kuleta mabadiliko, kama hii ya Uwezo imeonesha hali halisi ya matatizo katika elimu yetu, hivyo lisichukuliwe kisiasa na kuona kama ililenga kuidhalilisha serikali.”
Tunashauri wabunge kama Mariam Kasembe na pia viongozi wa serikali kuzingatia ushauri huo wa Balozi Mwapachu, na hali kadhalika, kwa upande mwingine tunawatia moyo HakiElimu na taasisi nyingine kama Uwezo kutokatishwa tamaa na kauli kama hizi.
No comments:
Post a Comment