Thursday, August 25, 2011

Wacha-Mungu anaoshauri Mwinyi waongoze nchi tunao?

HAMISI KIBARI
Dar es Salaam 

RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ametoa rai kwamba  nchi yetu  inatakiwa kuongozwa na viongozi wanaofuata maadili ya dini.
Mzee Mwinyi, alitoa kauli hiyo kwenye hafla ya mashindano ya kuhifadhi Qur’an Tukufu yaliyoshirikisha nchi 10 za Afrika. Mashindano hayo yaliyofanyika Dar es Salaam Jumapili iliyopita.

Katika hafla hiyo ambayo hata mimi niliishuhudia ikirushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Mzee Mwinyi alisema kwamba kiongozi mwenye maadili ya dini ataongoza kwa kumuogopa Mungu.

Mwinyi alisema: “Ili kuwapata viongozi waliokuwa wema na wenye kuongoza kwa usawa na haki, ni lazima watoke katika maadili ya kidini.” 

Rais huyo wa zamani alisema kwamba hata mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu wakuu wacha Mungu watafanya kazi yao kwa kumwogopa Mungu na njia mojawapo ya kuwapata ni kuhifadhi Qur’an Tukufu, kitabu ambacho pia kinataka miiko na mipaka anayopaswa kuwa nayo kiongozi wa umma. 

Kauli hiyo ya Rais wetu huyu mstaafu ambaye bila shaka kwa sasa anaona mengi, sawa na mchezaji ambaye anaweza kuona makosa zaidi anapotoka nje ya uwanja kuliko alivyokuwa ndani ya mechi, imenifikirisha sana hadi kuandika makala haya.

Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi

Mzee Mwinyi, ambaye alielezewa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama mtu muungwana na mpole wakati akimkabidhi uongozi wa nchi na kututaka tumpe kura zetu, bila shaka amekuwa akijionea namna ambavyo ufisadi umekuwa ukiitafuna nchi yetu. Ninaamini ukimrudisha madarakani leo anaweza kurekebisha mambo mengi hata yale ambayo hakuyaona wakati akiwa madarakani. Ikumbukwe kwamba, hata Mwalimu Nyerere wakati akiwa madarakani alikataza uwepo wa vyama vingi, lakini alijisahihisha na kuwa kinara wa kutaka vyama vingi virejee akiwa nje ya madaraka. Inaelezwa kwamba alikuwa pia anapigia debe uwepo wa wagombea binafsi ingawa katika utawala wake aliwapiga vita.

Mwinyi, kama tunavyoona sisi, naye anajionea watu tuliowakabidhi majukumu ya kutuongoza wakigeuka kuwa manyang’au hatari. Hawana huruma kabisa na Watanzania wenzao wanaotarajia neema ya raslimali hizi alizoziweka  Mwenyezi Mungu kwenye nchi yao ziwe chachu ya maendeleo yao. Kila kukicha ni wizi mtupu.

Mara utasikia nchi yetu imenunua rada kwa bei ya juu isivyo kawaida hadi waliotuibia wanatuonea huruma na kuturudishia chenji. Hujakaa sawa unasikia wakubwa wakijiuzia mgodi wao na familia zao kwa bei ya kutupwa. Ukiamka unasikia lingine kuhusu viongozi wetu hawa kutumia dharura ya mgawo wa umeme kuleta nchini kampuni ya kitapeli ili kula pesa za umma pasipo uhalali. Kabla hilo halijaisha, unasikia kwamba kumbe mikataba ya madini haitusaidii hata kuimarisha shilingi yetu wakati bei ya dhahabu duniani inapanda. Ukifungua televisheni yako kuwasikiliza wabunge unasikia mambo kadhaa yanayokuacha mdomo wazi; kwamba Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limeuzwa kinyemela na pesa kuingia kwenye akaunti za watu binafsi, kwamba kuna viongozi hawataki kusikia reli ya kati inaimarika kwa sababu wanapata faida wao binafsi kwa  kusafirisha mizigo kwa malori yao na kuifanya Tanzania iwe nchi pekee inayotumia usafiri ghali wa barabara na kushindwa kutumia manufaa ya bandari iliyojaaliwa na Mungu. Lakini lingine linaloshangaza, ni kusikia bungeni kwamba wanyama hai zaidi ya 100 walisafirishwa nje ya nchi kwa kutumia ndege 16 lakini serikali haikuingiza chochote kitu. Pale pale Bungeni unamsikia mbunge akiorodhesha watu waliomilikishwa ardhi kubwa katika mazingira yenye utata katika maeneo ya vijiji fulani huko wao wakiwa si wenyeji wa vijiji hivyo. Orodha ya majina, likiwemo la Mwinyi, inagusa majina ya vigogo tupu.

Hayo na mengine mengi, yanakuonesha kwamba viongozi wetu wengi hakuna wanachokiogopa pale wanapoamua kuiba. Hawajali kwamba ulafi huu wa kufaidi wao wenyewe na familia zao raslimali za Watanzania, wanasababisha vifo vingi vya Watanzania wanaokosa madawa mahospitalini kwa sababu ya uhaba wa fedha, wanaogua matumbo ya kuhara kutokana na kunywa maji yasiyo salama kwa sababu ya upungufu wa bajeti ya kuwapatia Watanzania wote maji safi na salama, kwamba uchumi wa nchi unayumba kutokana na serikali kulemewa na uwezo mdogo katika kuzalisha umeme wa uhakika na madhila mengine mengi.

Hawa wanajua mapesa wanayochukua si halali, ni ya umma wa Watanzania lakini kwa sababu hawamuogopi Mwenyezi Mungu, hawajui kama wana maswali ya kujibu mbele yake siku ya siku, na kwa kuwa wanaamini hakuna atakayewafanya lolote hapa duniani, wanaiba watakavyo.
Lakini, kwa nini Mwinyi anafikia hatua ya kukata tamaa na kututaka wananchi tuchague viongozi wacha Mungu ambao watajikuta wakijiwekea mipaka wao wenyewe katika matendo yao, yaani kumuogopa Mungu kila wanaposhawishika kutuibia?

Unaweza tena kujiuliza swali hili. Je, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi hajui kwamba nchi hii haina dini bali wananchi ndio wenye dini na hivyo Mtanzania yoyote ana haki ya kuchaguliwa kuwa kiongozi bila kujali kama ana dini ama hana? 

Mwinyi anapendekeza kwamba sifa ya kwanza kuwa kiongozi sasa iwe uchamungu wake, lakini swali lingine muhimu la kujiuliza ni hili: hao wacha Mungu wenyewe wanaomuogopa Mungu tunao? Je, Mwinyi ana taarifa zinazozidi kujitokeza kwamba baadhi ya wasafirishaji wakubwa wa madawa ya kulevya ambayo yanaumiza sana vijana wetu ni viongozi wa madhehebu ya dini?

Lakini bila shaka, kilichomfikisha hapo Mwinyi ni jinsi taifa letu linavyoenenda. Kwamba ufisadi umeshakuwa ‘fasheni’. Kila mtu kwa nafasi yake anatafuta kuukata kwa kuuibia umma wa Watanzania. Imefikia wakati mwizi wa mali ya umma, yaani anayetajirika haraka haraka kwa rushwa na ubadhirifu ndiye anaonekana kama mjanja.

Kwa lugha nyingine, wakati polisi wetu wakisumbuana na vibaka, majizi halisi yanayochangia maisha yetu Watanzania tulio wengi kuwa duni hayaguswi.

Mwinyi amejikatia tamaa kwa sababu sheria zetu ni kama zinawaona tu walalahoi wanaoiba kuku na simu kwenye vituo vya daladala na si wakubwa. Mwinyi bila shaka haoni pia mchango wowote kutoka kwa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika kudhibiti viongozi wasio na maadili. Bila shaka haoni pia mchango wa Sekreterieti ya Maadili ya Umma na ndio maana anatushauri sasa tuchague viongozi wachamungu. Mwinyi haoni pia ukaguzi unaofanywa kila mwaka na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ukifanyiwa kazi na serikali na kuzaa matunda, kwani yale yale anayoyagundua ni yale yale yanayojirudia kila mwaka. Amekata tamaa.

Ni ushauri mzuri sasa kuwageukia viongozi wacha Mungu, lakini kwa nini tufike huko? Kwa nini sheria zetu na taasisi zetu hazifanyi kazi sawasawa? Kwa nini hatusikii, kwa mfano, waliotuibia pesa zetu kupitia mradi wa rada wakifikishwa mahakamani? Waliojiuzia mgodi wa Kiwira kwa nini bado wako mitaani ama wale waliokwapua pesa za Epa kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture?

Nichukue fursa hii kumpiga kidogo dongo Rais Mstaafu Mwinyi kwamba yeye pia ni chanzo cha ufisadi huu unaoitesa nchi yetu kutokana na serikali aliyoiongoza kubariki Azimio la Zanzibar.
Azimio hili ambalo serikali ya Mwinyi ililipitisha kimya kimya, bila shaka kwa kujua kwamba lilikuwa na walakini, ndilo lililovunja miiko ya uongozi iliyowekwa awali na Azimio la Arusha. Azimio hilo, pamoja na mambo mengine lilimzuia mtu anayeshika madaraka katika ofisi ya umma kuwa na hisa katika makampuni binafsi.

Hakuna ubishi kwamba Azimio la Arusha lilikuwa sahihi kuwazuia viongozi wa umma kujihusisha na biashara ama kumiliki makampuni kwa sababu lilijua kuwa kuruhusu hilo ni kuruhusu watu kunajisi ofisi za umma kwa maslahi binafsi. 

Kimsingi serikali ya Awamu ya Nne ilishalijua hilo. Kumbukumbu zinaonesha kwamba Rais Jakaya Kikwete, mwaka 2008 aliwahi kueleza nia ya serikali yake kutunga sheria ya kuwazuia viongozi wa kisiasa kujihusisha na biashara. Kikwete alikuwa anahutubia Bunge baada ya kuunda baraza la mawaziri kufuatia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Dk. Ibrahim Msabaha (Afrika Mashariki) kujiuzulu.
Rais alisema kwamba kiongozi wa kisiasa ambaye ni mfanyabiashara anatakiwa kuamua moja, kutumikia umma ama kuendelea na biashara na si kuwatumikia mabwana hao wawili ili kuepuka migongano na kudhibiti mmomonyoko wa maadili.

Lakini inaonekana msimamo huo wa Rais haujafanyiwa kazi yoyote kwani wafanyabiashara, wakiwemo wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wameendelea kugombea nafasi za uongozi wa umma, huku wengine, yeye mwenyewe Kikwete akiwapigia debe wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Hata hivyo, mimi ninaamini kwamba Rais Kikwete ametupa rungu kwa kuruhusu uandishi wa Katiba mpya. Pengine ikiwa suluhisho la tatizo hili kama sisi wananchi tutakaa imara. Lazima suala la maadili na miiko ya uongozi lichukue nafasi kubwa katika Katiba hiyo mpya tunayotarajia kuiandika.

Si vibaya tukaiga mazuri ya katiba ya wenzetu wa Kenya ambao wamejitahidi kuliangalia kwa umakini suala la maadili na miiko ya uongozi. Baadhi ya mambo yanayovutia katika katiba yao ni kumpunguzia rais madaraka ya uteuzi wa nafasi nyeti na lingine ni pale kigogo, wakiwemo mawaziri, anapotajwa kwa tuhuma fulani, anawajibika kujiuzulu nafasi hiyo ili uchunguzi huru ufanyike juu yake.

Hii ni tofauti na huku kwetu ambapo katiba haielekezi utamaduni wa kujiuzulu kiasi kwamba vyama vya siasa ndivyo sasa vimeamua kuingilia kati, tena baada ya kuhisi kwamba vinapoteza umaarufu, kwa ‘kuwabembeleza’ wanachama wao wenye tuhuma za ufisadi kujiondoa madarakani wenyewe.

Hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuja na falsafa ya kujivua gamba, haitokani na huruma ambayo viongozi wa chama hicho wanayo kwa Watanzania, bali hofu ya kupoteza madaraka ya uongozi wa nchi kutokana na kupungua kwa umaarufu wa chama hicho. Hii inatokana na kunyooshewa kidole kwa muda mrefu kwamba baadhi ya wanachama wake walio watumishi wa umma ndio wanaoitafuna nchi kwa vitendo vyao vya ufisadi.

Lazima katiba tutakayoiandika iwabane kisawasawa wote watakaoshika ofisi za umma kujihusisha na biashara ama kuonekana wana mali kuliko mishahara yao. Tukiwa na katiba inayohimiza maadili na miiko ya uongozi, huku ikiruhusu wanaokiuka kushughulikiwa mara moja na taasisi zilizopo, bila shaka hatutofika anakotushauri Rais Mstaafu Mwinyi, yaani kila mara kuchagua wacha Mungu kuongoza nchi yetu ambao mimi ninadhani hatunao.

No comments:

Post a Comment