Thursday, August 25, 2011

TAHRIRI KULIKONI: HakiElimu, Uwezo msikatishwe tamaa



WAKATI wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Mbunge wa Jimbo la Masasi (CCM), Mariam Ruben Kasembe, alizishambulia tafiti mbalimbali zinazofanywa nchini na taasisi kama HakiElimu na kisha kutangazwa kwenye vyombo vya habari kuwa hazina maana yoyote zaidi ya kuidhalilisha serikali.

Mbunge huyo alidai kwamba wananchi hawayapendi matangazo ya HakiElimu, na hivyo akashauri eti ni heri pesa zinazotumika kwenye tafiti, machapisho na matangazo hayo zipelekwe kwenye maeneo husika yenye matatizo.

Mawazo ya mbunge huyu wa CCM hayana tofauti na yale ya wabunge wawili wa chama hicho ambao mwaka 2007 waliitaka serikali kuichukulia hatua HakiElimu kwa maelezo kuwa matangazo yake yamekuwa yakibeza juhudi za kuendeleza elimu nchini zinazofanywa na serikali. 

Wabunge walioonekana kukerwa na HakiElimu wakati wakichangia bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (2007), walikuwa Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa ambaye pia kwa sasa ni Naibu Spika na Janet Masaburi (Viti Maalumu).

Wakati Ndugai alidai kuwa matangazo hayo yanaweza kuiangusha serikali, Masaburi, alidai yanajenga chuki miongoni mwa wananchi dhidi ya serikali yao. 

Ikumbukwe pia kwamba serikali iliwahi kupiga marufuku matangazo ya asasi hiyo isiyo ya kiserikali na watu wengi walijitokeza kuitetea HakiElimu wakiishaanga serikali kwa hatua hiyo. Baadaye Serikali iliifungulia taasisi hiyo kuendelea na shughuli zake kama kawaida. 
Balozi Mwapachu

Tumeshindwa kujua kile ambacho kimekuwa kikiwakera wabunge wa CCM na hata serikali kuhusu ukweli unaowekwa wazi kwa njia ya machapisho na matangazo na taasisi ya HakiElimu na zingine za aina hiyo, kama Uwezo ambayo mapema mwaka huu ilitoa taarifa ya utafiti wake unaoonesha kuwa nchi yetu iko nyuma kielimu kulinganisha na wenzetu wa Kenya na Uganda.

Tunachojua sisi, machapisho ama matangazo yanayotolewa kwa njia ya maigizo na taasisi hizi hayaji kwa kukurupuka bali yanatokana na tafiti.  Kwa lugha nyingine, tafiti hizi tunazooneshwa kwa njia ya matangazo na machapisho zinalenga kutufumbua macho na kutuzindua kama taifa kuhusu hali halisi ilivyo ili tuchukue hatua na hivyo wahusika walitakiwa kupongezwa na si kubezwa, kutishwa ama kufungiwa.

Tunaandika haya tukijua kwamba nchi yetu bado ina kiwango kidogo sana cha tafiti na kwamba hatuwezi kuweka mipango yoyote ya maana ya maendeleo bila kusaidiwa na tafiti. 

Tunajua kwamba serikali imekuwa ikijitahidi kufanya maendeleo katika elimu lakini hiyo haimaanishi kwamba mambo kila siku yako shwari isipokuwa tafiti hizi ndizo zinatakiwa kuizindua serikali na jamii kwa ujumla ili kujua namna nzuri ya kutumia raslimali chache zilizopo kwa ajili ya maendeleo yetu.

Na tumeshindwa kujua kwa nini Mbunge Kasembe anawasingizia wananchi kwamba matangazo ya HakiElimu yanawaudhi, jambo ambalo tunaamini hajalifanyia utafiti. Matangazo ya HakiElimu yanaamsha hisia chanya kwa wananchi ili kuwawajibisha viongozi wao kuhusu cha kufanya kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya watoto wao.
Wakati akizindua taarifa ya taasisi ya Uwezo kuhusu utafiti wao mapema mwaka huu, Balozi Juma Mwapachu alisema kwamba tafiti hizi zinalenga kuangalia kwa kina matatizo yanayoikabili sekta ya elimu katika nchi yetu na namna ya kuyapatia ufumbuzi kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu.
Balozi Mwapachu alikaririwa akisema: “Ifike wakati tuzitumie tafiti hizi kuleta mabadiliko, kama hii ya Uwezo imeonesha hali halisi ya matatizo katika elimu yetu, hivyo lisichukuliwe kisiasa na kuona kama ililenga kuidhalilisha serikali.”
Tunashauri wabunge kama Mariam Kasembe na pia viongozi wa serikali kuzingatia ushauri huo wa Balozi Mwapachu, na hali kadhalika, kwa upande mwingine tunawatia moyo HakiElimu na taasisi nyingine kama Uwezo kutokatishwa tamaa na kauli kama hizi.

Wacha-Mungu anaoshauri Mwinyi waongoze nchi tunao?

HAMISI KIBARI
Dar es Salaam 

RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ametoa rai kwamba  nchi yetu  inatakiwa kuongozwa na viongozi wanaofuata maadili ya dini.
Mzee Mwinyi, alitoa kauli hiyo kwenye hafla ya mashindano ya kuhifadhi Qur’an Tukufu yaliyoshirikisha nchi 10 za Afrika. Mashindano hayo yaliyofanyika Dar es Salaam Jumapili iliyopita.

Katika hafla hiyo ambayo hata mimi niliishuhudia ikirushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Mzee Mwinyi alisema kwamba kiongozi mwenye maadili ya dini ataongoza kwa kumuogopa Mungu.

Mwinyi alisema: “Ili kuwapata viongozi waliokuwa wema na wenye kuongoza kwa usawa na haki, ni lazima watoke katika maadili ya kidini.” 

Rais huyo wa zamani alisema kwamba hata mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu wakuu wacha Mungu watafanya kazi yao kwa kumwogopa Mungu na njia mojawapo ya kuwapata ni kuhifadhi Qur’an Tukufu, kitabu ambacho pia kinataka miiko na mipaka anayopaswa kuwa nayo kiongozi wa umma. 

Kauli hiyo ya Rais wetu huyu mstaafu ambaye bila shaka kwa sasa anaona mengi, sawa na mchezaji ambaye anaweza kuona makosa zaidi anapotoka nje ya uwanja kuliko alivyokuwa ndani ya mechi, imenifikirisha sana hadi kuandika makala haya.

Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi

Mzee Mwinyi, ambaye alielezewa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama mtu muungwana na mpole wakati akimkabidhi uongozi wa nchi na kututaka tumpe kura zetu, bila shaka amekuwa akijionea namna ambavyo ufisadi umekuwa ukiitafuna nchi yetu. Ninaamini ukimrudisha madarakani leo anaweza kurekebisha mambo mengi hata yale ambayo hakuyaona wakati akiwa madarakani. Ikumbukwe kwamba, hata Mwalimu Nyerere wakati akiwa madarakani alikataza uwepo wa vyama vingi, lakini alijisahihisha na kuwa kinara wa kutaka vyama vingi virejee akiwa nje ya madaraka. Inaelezwa kwamba alikuwa pia anapigia debe uwepo wa wagombea binafsi ingawa katika utawala wake aliwapiga vita.

Mwinyi, kama tunavyoona sisi, naye anajionea watu tuliowakabidhi majukumu ya kutuongoza wakigeuka kuwa manyang’au hatari. Hawana huruma kabisa na Watanzania wenzao wanaotarajia neema ya raslimali hizi alizoziweka  Mwenyezi Mungu kwenye nchi yao ziwe chachu ya maendeleo yao. Kila kukicha ni wizi mtupu.

Mara utasikia nchi yetu imenunua rada kwa bei ya juu isivyo kawaida hadi waliotuibia wanatuonea huruma na kuturudishia chenji. Hujakaa sawa unasikia wakubwa wakijiuzia mgodi wao na familia zao kwa bei ya kutupwa. Ukiamka unasikia lingine kuhusu viongozi wetu hawa kutumia dharura ya mgawo wa umeme kuleta nchini kampuni ya kitapeli ili kula pesa za umma pasipo uhalali. Kabla hilo halijaisha, unasikia kwamba kumbe mikataba ya madini haitusaidii hata kuimarisha shilingi yetu wakati bei ya dhahabu duniani inapanda. Ukifungua televisheni yako kuwasikiliza wabunge unasikia mambo kadhaa yanayokuacha mdomo wazi; kwamba Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limeuzwa kinyemela na pesa kuingia kwenye akaunti za watu binafsi, kwamba kuna viongozi hawataki kusikia reli ya kati inaimarika kwa sababu wanapata faida wao binafsi kwa  kusafirisha mizigo kwa malori yao na kuifanya Tanzania iwe nchi pekee inayotumia usafiri ghali wa barabara na kushindwa kutumia manufaa ya bandari iliyojaaliwa na Mungu. Lakini lingine linaloshangaza, ni kusikia bungeni kwamba wanyama hai zaidi ya 100 walisafirishwa nje ya nchi kwa kutumia ndege 16 lakini serikali haikuingiza chochote kitu. Pale pale Bungeni unamsikia mbunge akiorodhesha watu waliomilikishwa ardhi kubwa katika mazingira yenye utata katika maeneo ya vijiji fulani huko wao wakiwa si wenyeji wa vijiji hivyo. Orodha ya majina, likiwemo la Mwinyi, inagusa majina ya vigogo tupu.

Hayo na mengine mengi, yanakuonesha kwamba viongozi wetu wengi hakuna wanachokiogopa pale wanapoamua kuiba. Hawajali kwamba ulafi huu wa kufaidi wao wenyewe na familia zao raslimali za Watanzania, wanasababisha vifo vingi vya Watanzania wanaokosa madawa mahospitalini kwa sababu ya uhaba wa fedha, wanaogua matumbo ya kuhara kutokana na kunywa maji yasiyo salama kwa sababu ya upungufu wa bajeti ya kuwapatia Watanzania wote maji safi na salama, kwamba uchumi wa nchi unayumba kutokana na serikali kulemewa na uwezo mdogo katika kuzalisha umeme wa uhakika na madhila mengine mengi.

Hawa wanajua mapesa wanayochukua si halali, ni ya umma wa Watanzania lakini kwa sababu hawamuogopi Mwenyezi Mungu, hawajui kama wana maswali ya kujibu mbele yake siku ya siku, na kwa kuwa wanaamini hakuna atakayewafanya lolote hapa duniani, wanaiba watakavyo.
Lakini, kwa nini Mwinyi anafikia hatua ya kukata tamaa na kututaka wananchi tuchague viongozi wacha Mungu ambao watajikuta wakijiwekea mipaka wao wenyewe katika matendo yao, yaani kumuogopa Mungu kila wanaposhawishika kutuibia?

Unaweza tena kujiuliza swali hili. Je, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi hajui kwamba nchi hii haina dini bali wananchi ndio wenye dini na hivyo Mtanzania yoyote ana haki ya kuchaguliwa kuwa kiongozi bila kujali kama ana dini ama hana? 

Mwinyi anapendekeza kwamba sifa ya kwanza kuwa kiongozi sasa iwe uchamungu wake, lakini swali lingine muhimu la kujiuliza ni hili: hao wacha Mungu wenyewe wanaomuogopa Mungu tunao? Je, Mwinyi ana taarifa zinazozidi kujitokeza kwamba baadhi ya wasafirishaji wakubwa wa madawa ya kulevya ambayo yanaumiza sana vijana wetu ni viongozi wa madhehebu ya dini?

Lakini bila shaka, kilichomfikisha hapo Mwinyi ni jinsi taifa letu linavyoenenda. Kwamba ufisadi umeshakuwa ‘fasheni’. Kila mtu kwa nafasi yake anatafuta kuukata kwa kuuibia umma wa Watanzania. Imefikia wakati mwizi wa mali ya umma, yaani anayetajirika haraka haraka kwa rushwa na ubadhirifu ndiye anaonekana kama mjanja.

Kwa lugha nyingine, wakati polisi wetu wakisumbuana na vibaka, majizi halisi yanayochangia maisha yetu Watanzania tulio wengi kuwa duni hayaguswi.

Mwinyi amejikatia tamaa kwa sababu sheria zetu ni kama zinawaona tu walalahoi wanaoiba kuku na simu kwenye vituo vya daladala na si wakubwa. Mwinyi bila shaka haoni pia mchango wowote kutoka kwa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika kudhibiti viongozi wasio na maadili. Bila shaka haoni pia mchango wa Sekreterieti ya Maadili ya Umma na ndio maana anatushauri sasa tuchague viongozi wachamungu. Mwinyi haoni pia ukaguzi unaofanywa kila mwaka na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ukifanyiwa kazi na serikali na kuzaa matunda, kwani yale yale anayoyagundua ni yale yale yanayojirudia kila mwaka. Amekata tamaa.

Ni ushauri mzuri sasa kuwageukia viongozi wacha Mungu, lakini kwa nini tufike huko? Kwa nini sheria zetu na taasisi zetu hazifanyi kazi sawasawa? Kwa nini hatusikii, kwa mfano, waliotuibia pesa zetu kupitia mradi wa rada wakifikishwa mahakamani? Waliojiuzia mgodi wa Kiwira kwa nini bado wako mitaani ama wale waliokwapua pesa za Epa kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture?

Nichukue fursa hii kumpiga kidogo dongo Rais Mstaafu Mwinyi kwamba yeye pia ni chanzo cha ufisadi huu unaoitesa nchi yetu kutokana na serikali aliyoiongoza kubariki Azimio la Zanzibar.
Azimio hili ambalo serikali ya Mwinyi ililipitisha kimya kimya, bila shaka kwa kujua kwamba lilikuwa na walakini, ndilo lililovunja miiko ya uongozi iliyowekwa awali na Azimio la Arusha. Azimio hilo, pamoja na mambo mengine lilimzuia mtu anayeshika madaraka katika ofisi ya umma kuwa na hisa katika makampuni binafsi.

Hakuna ubishi kwamba Azimio la Arusha lilikuwa sahihi kuwazuia viongozi wa umma kujihusisha na biashara ama kumiliki makampuni kwa sababu lilijua kuwa kuruhusu hilo ni kuruhusu watu kunajisi ofisi za umma kwa maslahi binafsi. 

Kimsingi serikali ya Awamu ya Nne ilishalijua hilo. Kumbukumbu zinaonesha kwamba Rais Jakaya Kikwete, mwaka 2008 aliwahi kueleza nia ya serikali yake kutunga sheria ya kuwazuia viongozi wa kisiasa kujihusisha na biashara. Kikwete alikuwa anahutubia Bunge baada ya kuunda baraza la mawaziri kufuatia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Dk. Ibrahim Msabaha (Afrika Mashariki) kujiuzulu.
Rais alisema kwamba kiongozi wa kisiasa ambaye ni mfanyabiashara anatakiwa kuamua moja, kutumikia umma ama kuendelea na biashara na si kuwatumikia mabwana hao wawili ili kuepuka migongano na kudhibiti mmomonyoko wa maadili.

Lakini inaonekana msimamo huo wa Rais haujafanyiwa kazi yoyote kwani wafanyabiashara, wakiwemo wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wameendelea kugombea nafasi za uongozi wa umma, huku wengine, yeye mwenyewe Kikwete akiwapigia debe wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Hata hivyo, mimi ninaamini kwamba Rais Kikwete ametupa rungu kwa kuruhusu uandishi wa Katiba mpya. Pengine ikiwa suluhisho la tatizo hili kama sisi wananchi tutakaa imara. Lazima suala la maadili na miiko ya uongozi lichukue nafasi kubwa katika Katiba hiyo mpya tunayotarajia kuiandika.

Si vibaya tukaiga mazuri ya katiba ya wenzetu wa Kenya ambao wamejitahidi kuliangalia kwa umakini suala la maadili na miiko ya uongozi. Baadhi ya mambo yanayovutia katika katiba yao ni kumpunguzia rais madaraka ya uteuzi wa nafasi nyeti na lingine ni pale kigogo, wakiwemo mawaziri, anapotajwa kwa tuhuma fulani, anawajibika kujiuzulu nafasi hiyo ili uchunguzi huru ufanyike juu yake.

Hii ni tofauti na huku kwetu ambapo katiba haielekezi utamaduni wa kujiuzulu kiasi kwamba vyama vya siasa ndivyo sasa vimeamua kuingilia kati, tena baada ya kuhisi kwamba vinapoteza umaarufu, kwa ‘kuwabembeleza’ wanachama wao wenye tuhuma za ufisadi kujiondoa madarakani wenyewe.

Hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuja na falsafa ya kujivua gamba, haitokani na huruma ambayo viongozi wa chama hicho wanayo kwa Watanzania, bali hofu ya kupoteza madaraka ya uongozi wa nchi kutokana na kupungua kwa umaarufu wa chama hicho. Hii inatokana na kunyooshewa kidole kwa muda mrefu kwamba baadhi ya wanachama wake walio watumishi wa umma ndio wanaoitafuna nchi kwa vitendo vyao vya ufisadi.

Lazima katiba tutakayoiandika iwabane kisawasawa wote watakaoshika ofisi za umma kujihusisha na biashara ama kuonekana wana mali kuliko mishahara yao. Tukiwa na katiba inayohimiza maadili na miiko ya uongozi, huku ikiruhusu wanaokiuka kushughulikiwa mara moja na taasisi zilizopo, bila shaka hatutofika anakotushauri Rais Mstaafu Mwinyi, yaani kila mara kuchagua wacha Mungu kuongoza nchi yetu ambao mimi ninadhani hatunao.

Tusifananishe ya Libya na yaliyojiri Misri, Tunisia

 

HAMISI KIBARI
Dar es Salaam

Kanali Muammar Gddafi
WAKATI niliposikia maandamano yameibuka nchini Libya ya kutaka kumuondoa madarakani Kanali Muammar Gadaffi aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 42, niliunganisha na yale yaliyoziangusha serikali za Misri na Tunisia.
Kama walivyo Watanzania wengi, nilichukulia kwamba ni wimbi la mageuzi yanayotokana na nguvu ya umma katika nchi za Kiarabu baada ya watawala wake kung’ang’ania madaraka kwa muda mrefu. Nchi nyingine za Kiarabu zinazokumbwa na machafuko ni Yemen, Bahrain na Syria.
Kama walivyo wapenda demokrasia wengi duniani, hakuna anayependa kuona mtu mmoja anataka kutawala milele na huku akiandaa wanawe kumrithi na kutaka kujenga utawala wa kifalme. Kwa msingi huo, nilianza kuunga mkono juhudi za kumng’oa Gadaffi madarakani.
Lakini kadri siku zilivyokwenda, taratibu nilianza kushituka. Niligundua kwamba yanayotokea Libya si mapambano ya nguvu ya umma, bali kuna uasi. Yaani wale wanaoandamana wanatumia silaha za moto kutaka kumng’oa madarakani Gadaffi tofauti na tulivyokuwa tunaaminishwa, na hususan kupitia vyombo vya habari vya Magharibi.
Nilitilia shaka zaidi hali inayotokea Libya kutokana na waasi kuungwa mkono na ubeberu wa nchi za Magharibi ukiongozwa na Marekani.
Mwanzoni tulisikia kutolewa kwa Azimio la Umoja wa Mataifa (UN) lililodai kwamba Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi (Nato) sambamba na Marekani wanaanzisha operesheni tu ya kibinadamu nchini Libya. Yaani tulichoaminishwa kujua ni kwamba majeshi ya Gaddafi yanakiuka haki za msingi za raia ikiwa ni pamoja na kuua watu na hivyo Nato ilikuwa inaingia pale kwa lengo la kuwahami wananchi wasio na silaha dhidi ya utawala dhalimu.
Lakini kilichokuja kujitokeza baadaye ni kwamba mapigano yale nchini Libya ni ya Nato kwa mgongo wa waasi, yakiwa na lengo la kubadilisha uongozi na si kuwahami raia.
Kingine kinachotia kichefuchefu ni Nato kutotaka kusikiliza ushauri wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) ambao ulionekana ukitafuta suluhu bila kumwaga damu zaidi lakini Nato haikutaka kuwasililiza. Na hii kwa kweli ni udhalilishaji wa viongozi wetu wa Afrika.
Kadhalika, Gaddafi aliwahi kukaririwa kutaka mazungumzo na waasi katika kuamua mustakabali wa nchi hiyo, lakini waasi walikataa katakata. Nia yao ni lazima Gaddafi aondoke, si kwa sanduku la kura bali kwa mtutu.

Nilibahatika kuongea na kijana mmoja Raia wa Libya anayesoma Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akanisimulia kwa kifupi mtazamo wake na mapigamo katika nchi yao. Yeye anamuunga mkono Gaddafi na alijibu maswali yangu na wengine tuliokuwepo tukimsikiliza. Kwa kweli kijana huyu wa Libya, ameongeza mtazamo wangu kuwa hasi zaidi dhidi ya ubeberu unaofanywa na nchi za Magharibi na Marekani dhidi ya Afrika. Kiasi kwamba ninawaomba wachambuzi wenzangu wakati tunapoliangalia suala la Libya, tujue pia kwamba hapa kuna ubeberu: Maswali yetu dhidi ya kijana huyu kutoka Libya aliyeko Tanzania na ambaye anamuunga mkono Gaddafi yalikuwa namna hii:
SWALI: Kwa nini unawapinga waasi?
YEYE: Unajua waasi asili yao wanatokea katika mjini wa Benghazi. Hapa ni kwao aliyekuwa kiongozi wa Libya aliyepinduliwa na Gaddafi. Siku zote watu wa Benghazi wamekuwa hawaridhiki na utawala wa Gaddafi, siyo kwamba hauna mafanikio bali ni kwa sababu wanaamini kwamba lazima wao ndio watawale Libya. Kwa hiyo utaona kwamba hawapigani si kwa sababu nyingine isipokuwa uroho tu wa madaraka.
SWALI: Lakini Gaddafi analaumiwa kwa udikteta na kutaka kufia madarakani, kwa maana kwamba haruhusu demokrasia ishamiri nchini Libya. Unasemaje?
YEYE: Huo ndio mtazamo wa wengi hasa huku Tanzania na kwingineko. Mbaya zaidi wengi mnalishwa taarifa za Kimagharibi ambazo hazina ukweli wowote. Lakini ninachojua mimi Gaddafi si rais na wala haongozi nchi kibabe. Katika nchi yetu ameruhusu watu kushiriki katika mabaraza na kuamua mustakabali wa mambo yao na yeye haingilii kati. Wananchi wakiamua kwamba Waziri fulani hafai ama ameshindwa kutekeleza hili ama lile lazima aondoke madarakani, si kama hapa Tanzania nimeona waziri si rahisi kuondolewa madarakani kwa nguvu ya wananchi.
SWALI: Kwa hiyo wewe ungependa Gaddafi aendelee kutawala milele?
YEYE: Sina jibu la moja kwa moja lakini ukweli ni kwamba Gaddafi ametufanyia mengi watu wa Libya ambayo ninaamini hakuna mtawala atakayeweza kufikia alikofika.
Unajua nchi yetu ni Jangwa, na ukisikia maisha yalivyokuwa kabla ya kuja kwa Gaddafi madarakani utashangaa sana. Kulikuwa na umaskini wa kutisha. Lakini serikali ya Gaddafi ni serikali inayowajali wananchi kuliko serikali yoyote duniani ambayo mimi ninaifahamu. Kwanza katika nchi yetu, licha ya kuwa ni jangwa, hakuna taabu ya maji kama hapa Tanzania, mkate ni bei rahisi sana kama shilingi 250 tu ya Tanzania, sukari ni rahisi, elimu na matibabu ni bure. Watu wanaotaka kuoa na hawana uwezo wanalipiwa na serikali mahari na kupatiwa msingi wa maisha. Watoto wote yatima ni mali ya serikali. Si rahisi kuona chokoraa (watoto wa mitaani) kama huku kwenu Tanzania.
SWALI: Lakini, pamoja na kufanya yote hayo,  Gaddafi anadaiwa kujilimbikizia mali kibao nje ya nchi. Unasemaje kuhusu hilo?
YEYE: Mimi ninadhani ni propaganda tu za Kimagharibi. Ninaamini hizo ni pesa za serikali zinatokana na mafuta. Kwa sababu mafuta hayauzwi kama kanzu dukani, kwamba ukiuza unalipwa hapo hapo. Mimi ninaweza kusema hata kama Gaddafi amejitunzia mapesa huko nje, wacha ajitunzie kwa sababu wakati anaingia madarakani hakukuta kitu lakini kasimamia uchumi vizuri kiasi kwamba hatuombiombi nje kama wengine na hakuna mwananchi anayelalamika kwamba serikali imeshindwa kufanya hili ama lile.
Ninaweza kusema Libya kama hakuna mikataba mibovu kama ninayosikia katika nchi nyingine ikiwemo hapa Tanzania. Raslimali zetu tunazifaidi Walibya. Mimi ninaamini hili linawaudhi sana mabeberu wa Magharibi ambao wanapenda sana kutunyonya Waafrika.
Kinachowasumbua waasi ni chuki tu kwa sababu wanaamini kwamba mtawala lazima atoke Benghazi na siyo Tripoli.
SWALI: Lakini tunaona waasi wakishangiliwa na wananchi kwa kukomboa maeneo. Unasemaje?
YEYE: Kwanza usiite kukomboa bali ni kuyateka. Kinachofanyika ni propaganda tu za vyombo vya habari vya Magharibi. Mimi ninawasiliana na marafiki zangu, ndugu zangu karibu kila sehemu nyumbani Libya, lakini wote hawaonekani kuwaunga mkono waasi. Kile kinachofanyika ni kwamba waasi wanapiga sehemu, hata kama ni mbali na mji, kisha wanaita waandishi wao na kutangaza kile ambacho ulimwengu unatakiwa kujua na si ukweli halisi wa mambo. Yaani kwa kweli ukisoma habari za vyombo vya Magharibi na kusikia wananchi wanavyosema ni vitu viwili tofauti. Nyinyi hamwezi kuona uongo wa waasi walivyodai majuzi kwamba wamewateka watoto wa Gaddafi lakini baada ya muda ikagundulika kwamba ni uongo mtupu.
Ninachoweza kusema ni kwamba kinachotuponza Libya ni msimamo wa Gaddafi wa kupinga unyonyaji wa Magharibi. Wanachotafuta kwetu ni mafuta yetu basi. Kwa nini hamjiulizi kwamba Nato hawakupeleka majeshi Misri, Syria wala Tunisia? Kwa mfano wanadai Gaddafi anaua raia kwani hamjui Hosni Mubaraka wa Misri anashitakiwa kwa serikali yake kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wakimpinga? Mbona Nato hawakupeleka majeshi? Je, mnasemaje kuhusu Syria, mbona hakuna majeshi ya Nato? Yaani tunadanganywa sana Waafrika.
SWALI: Unazungumziaje majaaliwa ya Libya?
YEYE: Ninajua mpaka sasa wanapiga sana Tripoli lakini majeshi ya Gaddafi bado yako imara. Lakini lolote linaweza kutokea lakini ninajua si muda mrefu Walibya tutaikumbuka neema ya Gaddafi. Mimi ninaombea ushindi kwa Gaddafi.

Monday, January 31, 2011

Mjadala wa Katiba mpya hautazimwa

 Prof. Issa Shivji

 Jenerali Ulimwengu

 Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

HAMISI KIBARI

MWANZONI mwa wiki hii, gazeti moja limemkariri Mbunge wa Monduli, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akitoa tahadhari kwamba mjadala kuhusu Katiba mpya usiwe chanzo cha kuharibu amani iliyoko nchini. 

Kwa mujibu wa gazeti moja litokalo kila siku, Lowassa alisema kwamba kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo eti moyo wa kuharibika kwa amani unavyozidi kuongezeka nchini.
Akakaririwa akisema kwamba eti  katika mijadala mbalimbali inayoendelea nchini, hasa ya Katiba, wananchi wanatakiwa kupingana kwa hoja na si kwa kuhatarisha amani.
Lowassa pia aliwashauri waimbaji wa Injili kutunga nyimbo zinazohamasisha na kuchochea utunzaji wa amani, ili iendelee kudumu. 

 “Hakikisheni mnatunga nyimbo za kutetea amani maana kwa sasa kila mtu ana lake analosema, vyombo vya habari vinachochea kwa njia yake, hivyo tuilinde hii amani,” alikaririwa akisema sentensi hiyo.

Ni kweli, tunahitaji kuona watu wakikemea mambo ambayo yanaweza kuhatarisha kuvunjika kwa amani tunayojivunia. Lakini swali la kujiuliza hapa ni hili; kweli mjadala kuhusu katiba mpya unaoendelea nchini kote, kuanzia kwenye majukwaa ya siasa, makanisani na misikitini hadi kwenye vijiwe vya kahawa una dalili yoyote ya kuvunja amani ama ni kuiokoa Tanzania isielekee kwenye kuvunjika kwa amani kama ilivyotokea kwa majirani zatu wa Kenya

Tunaambiwa kwamba  Lowassa alitoa (tahadhari?) hii wakati akifungua Studio ya muziki iiitwayo FLEM ya jijijini Dar es Salaam, lakini mimi ninajiuliza tena swali hili; Waziri Mkuu huyu wa zamani alikosa la kusema siku hiyo?

Lowassa alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku takriban moja baada ya wanazuoni, wanasiasa na wanaharakati kukutana chuo kikuu cha Dar es Salaam kujadili na kupendekeza namna mchakato wa kuandika Katiba mpya unavyopaswa kufanyika.

Tangu nisome habari hiyo, nimekuwa ninajiuliza maswali kadhaa bila majibu ikiwa ni pamoja na haya; Je, Lowassa ameona wapi mjadala huu ukiwa na dalilia za uvunjifu wa amani ama ni yeye anayepandikiza kitu kingine ambacho sisi wengine hatukioni? 

Je, yeye hajayaona maeneo yenye dalili za kuvunja amani ya nchi yetu ambako alitakiwa kuharakisha kutoa kauli kama hizi?

Ninasikia aliwahi kutoa ushauri ambao ungeweza kuepusha vurugu za Arusha kama ungefanyiwa kazi kwa kutaka pande zilizokuwa kwenye mzozo kukutana kabla ya kilichotokea, lakini baada ya vurugu kutokea na kusababisha mauaji amesema nini? Je, kwa nini asilingetumia jukwaa la FLEM kuwasuta hao walioshindwa kutumia ushauri wake ili kuzuia yaliyotokea badala ya kuamua ‘kuuza sura’ akiongea ‘pumba’.

Je, wakati ule Tume ya Uchaguzi ya Taifa ilipokuwa inachelewesha kutoa matokeo huku ukweli ukiwa umeshabainika mshindi ni nani katika majimbo kwa sababu kura zilikuwa zinabandikwa kila kituo, alikuwa wapi kutoa kauli za kukemea hali kama hiyo kwa sababu inahatarisha amani ya nchi?

Ninachojua mimi, kama nitakavyoeleza hapa chini, wanaojadili umuhimu wa kuandikwa kwa Katiba mpya sasa ndio wanaoitakia mema nchi yetu iondokane na kuvunjika kwa amani siku moja. Hawa ni kuanzia watu wenye heshima katika jamii yetu kwa kufanya kazi zilizotukuka kama vile Jaji mstaafu Dk. Robert Kisanga, Jaji Mark Bomani, Profesa Issa Shivji, Jenerali Ulimwengu, Mwanasheria Mabere Marando, Dk. Benson Bana na wengineo.

Je, ni kweli Lowassa hajui kwamba msingi mkuu wa kilichotokea Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na kusababisha muaji ya takriban watu 1000 na wengine zaidi ya laki sita kukimbia makazi yao ni ubovu wa katiba? Je, hajui kwamba baada ya Kenya kuja na katiba mpya sababu zilizosababisha mauaji ya Kenya na ambazo zinaweza kutokea hapa kwetu wao wameondokana nazo?

Kwa kifupi ni kwamba sisi Tanzania tumeendelea kuwa na Tume isiyoonekana kuaminika na pande zote mbili, chama tawala na upinzani huku pia Katiba ikiwa hairuhusu kupinga uchaguzi wa rais wa mahakamani baada ya kutangazwa. Je, kadri wananchi wanavyozidi kujua haki zao hilo pekee la kutohoji uhalali wa kura za rais haliwezi kutupeleka pabaya siku moja?

Mimi nadhani Lowassa alipaswa kuwahamasisha makada wenzake katika CCM kuchangamkia mjadala wa uandikwaji wa katiba mpya kama anaitakia mema nchi yetu hata kama anadhani katiba iliyopo sasa inawabeba CCM kwa vile bado imejengwa katika mfumo wa chama kimoja.
Ninasema hivyo nikiwa nina habari kwamba wabunge na viongozi wengine wa chama tawala hatukuwaona katika kongamano lile la chuo kikuu kuhusu Katiba Mpya lililotayarishwa na Jumuiya ya wanataaluma wa chuo hicho (Udasa).

Hebu tuangalie kwa kifupi yaliyojiri kwenye kongamano hilo la Jumamosi iliyopita kama kweli yaneweza kuhatarisha amani ama kusaidia kuijenga: Profesa Issa Shivji ambaye alikuwa mmoja wa watoa mada, alisema kwamba wakati sasa umefika kwa wananchi wa Tanzania kuwa na katiba mpya ambayo itajumuisha misingi ya taifa itakayokuwa imelinda maslahi ya wananchi.
Tena akasema suala hilo lisiachwe kwa wanasiasa (kama Lowassa)  kwani katiba mpya inapaswa iangalie maslahi ya walio wengi na hasa wanaoishi vijijini kwa kuangalia ardhi, madini, wanyama na maliasili nyingine. Pia alisema  Katiba hiyo inapaswa kuangalia mfumo mzima wa serikali kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi.
Je, mjadala kama huo ambao  Jenerali Ulimwengu, alisema wakati umefika kwa wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya kwa kuwa historia inaonyesha kwamba mabadiliko ya katiba yaliyofanywa huko nyuma hawakushirikishwa unavujanje amani kwa mujibu wa mtazamo wa Lowassa?
Hata mimi ninakubaliana na Jenerali alivyosema; “Wakati umefika kwa raia kuwa na nafasi juu ya serikali yao na siyo serikali kuwa na nafasi juu ya wananchi. Ni fursa ya kujiangalia upya na tusikubali kwenda haraka haraka; si zoezi la Rais, Bunge, vyama vya siasa, wanazuoni au waandishi wa habari, ni la Watanzania wote.”
Hivi Lowassa angetaka mjadala wa katiba mpya ufanywe na akina nani ili aone kwamba hakuna uvujifu wa amani… Makada wa CCM ambao wanakimbia maeneo kama haya? 
Kweli mtu kama Lowassa anaweza kukubaliana na pendekezo alilolitoa Jenerali kwamba mjadala kuhusu mchakato wa katiba mpya uanze ndani ya vyama vya kiraia, kuona namna ya kuboresha misingi itakayolinda masilahi ya wananchi ili wawe na usemi kuhusu raslimali zao na serikali yao
Lowassa huyu tunayemfahamu, ambaye hakuachia ngazi ya nafasi ya Uwaziri Mkuu kwa moyo mmoja inatia shaka kama anaweza kufurahia ushauri kama huu ulioendelea kutolewa na Jnerali Ulimwengu katika kongamano hilo kwamba mchakato wa kuandika Katiba mpya utaisaidia Tanzania kujisanifu upya kwa kutambua rasilimali zote za taifa zilizo chini na juu ya ardhi na kuainisha umiliki na matumizi yake.
Jenerali alisema kwa usanifu huo, taifa litaweka bayana nani mwenye mamlaka ya kuruhusu matumizi ya rasilimali hizo na kwa wakati gani kuliko ilivyo katika katiba ya sasa.
Mimi binafsi, ninaaamini kama alivyosema mbunge wa Iramba Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kwenye kongamano hilo kwamba katiba iliyopo hivi sasa haiwezi tena kutumika kwa kuwa ina makosa mengi ambayo hayawezi kuendelea kuvumiliwa.
Ninaamini hata Lowassa anajua kwamba jambo moja kubwa ambalo haliwezi kuendelea kuvumilika ni katiba hii kuendelea kukibeba chama tawala, katika mfumo huu wa vyama vingi unaoruhusiwa na katiba hiyo hiyo. Mambo mengine ni Rais kuendelea kuwa na madaraka makubwa huku wananchi wakiwa hawana uwezo wa kuamua na kuhoji kuhusu matumizi ya raslimali zao (hata kama ni kwa kupitia wawakilishi wao, yaani wabunge).
Ninamtaka pia Lowassa ajue kwamba sisi wananchi tunaojadili katiba mpya katika kipindi hiki cha amani badala ya kusbiri mambo yaharabike kama ilivyotokea Kenya tunaamini kwamba tumaini letu kubwa katika kulinda uhuru wetu na kushuhudia anguko la mafisadi na viongozi wasiofaa ni katiba mpya.
Wananchi tumechoka kuendelea kuona watu wachafu wakinunua uongozi na kusimama kwenye majukwaa wakipigiwa makofi badala ya kuwa jela kutokana na kuwaibia Watanzania raslimali zao kila kukicha.
Wananchi tumechoka na watu waliogeuza siasa kuwa mradi mkubwa wa kuwatajirisha wao na familia zao kwa njia za mkato na kuuacha umma mkubwa wa Watanzania ukitopea katika lindi la umaskini.
Na nionavyo mimi, moto wa mageuzi ya katiba hauwezi kuzimwa na kauli rejareja kama hizi za Lowassa ama wengine wenye matazamo kama wake.
Kadhalika, nionavyo mimi Watanzania kwa asili yao ama walivyojengwa na tawala zilizopita, hususan enzi za Mwalimu Julius Nyerere ni wapenda amani na ndio mana wamekuwa wakifumbia madudu mengi sana kama vile hawaoni likiwemo la kunyimwa haki ya kupinga uchaguzi wa rais mahakamani. Yapo mambo yanayowakera sana watanzania, kubwa likiwa ni ufisadi unaosababisha raslimali zao kuporwa na wajanja wachache. Kama ndivyo, na kama ana ubavu, hayo ndiyo mambo ambayo Lowassa alitakiwa kuwaambia waimba Injili watunge nyimbo za kuyakemea badala ya kuwataka eti kukemea amani ambayo tunayo na halijawa tatizo kiasi hicho. Au Lowassa hana ubavu (moral authority) wa kuwataka waimba Injili sasa kulipuka na nyimbo kila kona wakikemea ufisadi?!!
Lowassa pia amevihusisha vyombo vya habari kwa kudai kuchochea kuvurugika kwa amani kupitia mjadala wa katiba kitu ambacho pia kinashangaza. Ninavyojua mimi vyombo vingi vya habari, ukiachilia mbali vya marafiki zake wanaomuunga mkono, vinapigania maslahi ya nchi ambayo pengine kwa Lowassa anaona kama ni kuvuruga amani. Vyombo vya habari likiwemo gazeti hili vimejitahidi kuonyesha uzalendo wa kweli kwa nchi yetu.
Vyombo vya habari vinavyotetea mafisadi na ufisadi, kama anaweza, ndivyo alivyopaswa kuvinyooshea kidole kwanza na hivi ndivo, kwa mtazamo wangu, vinavyokejeli mijadala yenye manufaa kwa nchi yetu.

Mwandishi ni Mhariri wa gazeti hili. Unaweza kuwasiliana naye kupitia  Email: hkibari1965@gmail.com au simu 0713328006/0758 143457/ 0789328006