MAKALA


Wananchi wakiwa wamejaza kwenye treni

MPANGO WA KUFUFUA RELI YA KATI...
Tunawajua maadui watakaosababisha isinyanyuke?

HAMISI KIBARI

IKO kampuni moja binafsi, inaelezwa kwamba maofisa wake fulani walikuwa wanashirikiana na ‘vishoka’ wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kukata maji kwa makusudi ili yasifike katika majengo ya kampuni hiyo.

Kwa vile ni lazima kampuni hiyo itumie maji kwa siku kwa ajili ya kuendeshea shughuli za uzalishaji na huduma nyingine kama za choo, ilikuwa inalizimika kununua maji kwa maelezo kwamba maji hayafiki katika ofisi hiyo ambayo nimeamua kuficha jina lake kwa sababu zangu binafsi.

Kwa kununua maji kwenye magari yenye matenki, maofisa hao wachache walikuwa wanagawana na madereva wa magari hayo kiasi fulani cha fedha zinazolipwa na kampuni, fedha ambazo kimsingi ni wizi mtupu.

Kabla ya ujanja huo kugundulika, kila mara kampuni ilipokuwa inafanya juhudi za kutaka kushughulikia tatizo la maji kufika katika majengo ya kampuni, wajanja waliokuwa wanakata maji makusudi na kufaidi hali hiyo walikuwa wanaweka vikwazo hivi na vile.

Kuna madai mengine yanayofanana na utangulizi huo (ingawa nikiri kuwa sina uhakika nayo sana) kwamba baadhi ya magonjwa fulanifulani yangeliweza kutibika hapa Tanzania kwa sababu tayari wataalamu wapo na wamesomeshwa kwa kodi zetu hizi. Mbali na hilo, inasemekana kwamba tayari zipo hata hospitali binafsi zingeweza kutibu maradhi hayo hapa hapa nchini kwa sababu zina wataalamu na vifaa.

Lakini kwa mshangao wa wengi kila mwaka wenye magonjwa hayo wanaendelea kupelekwa nje, hususan India na juhudi zozote za kutaka magonjwa hayo yatibiwe nchini zinapigwa sana vita.

Kwa nini zinapigwa vita, inadaiwa kwamba ni kwa sababu kwa kupeleka wagonjwa nje, kipo kikundi cha watu fulani kinafaidi. Yaani kina maslahi binafsi juu ya hilo na kinapiga vita kwa nguvu zao zote juhudi zozote za kuua mrija wao huo. Inadaiwa kwamba hata hospitali binafsi zinazodai kuwa na uwezo wa kutibu magonjwa hayo hazitakiwi kabisa machoni mwa watu hao.

Yapo pia madai kwamba katika nchi yetu kuna watu wanafaidika sana na mgawo wa umeme kama huu unaoendelea nchini kote. Na kama kuna kitu wanaofaidi mgawo hawataki kukisikia ni kauli kwamba “serikali itamaliza kabisa mgawo wa umeme ifikapo tarehe ama mwaka fulani”.

Yaani, licha ya mgawo wa umeme kuvuruga uchumi wa nchi, kusababisha Watanzania kadhaa kukosa ajira na madhila mengine mengi, lakini alimradi wao binafsi na familia zao wanafaidi, wanapiga vita juhudi zozote za kumaliza mgawo wa umeme nchini. Hali kadhalika wanaomba dua usiku na mchana Mungu ajaalie hali hii mbaya kwa walio wengi iendelee.

Yapo madai kwamba wapo watu hawa wanafaidi mgawo wa umeme kwani unawawezesha kuibuka na miradi feki ya dharura ya kumaliza tatizo la umeme kama ule wa Richmond/Dowans. Inadaiwa pia kwamba wapo maofisa wanaotumia mwanya huu wa mgawo wa umeme kufaidi pesa za kununua mafuta kwenye majenereta wanayolazimika kuyawasha kwenye makampuni yao, zikiwemo idara kadhaa nyeti za umma.

Wapo wanaokwenda mbali na kudai kwamba hata ule mradi maarufu wa Stieglers Gorge unapigwa vita kwa sababu ukifanikishwa utasababisha tatizo la umeme kuwa historia. Inaelezwa kwamba mradi huo wenye uhakika wa kuipa Tanzania megawati zaidi ya 2000 (yaani zaidi ya mara mbili ya miradi yote inayozalisha umeme kwa sasa), ni mradi wa umeme rahisi wa maji ulio katika bonde la Mto Rufiji linaloaminika kwamba ni nadra kupungua maji kama serikali itasamamia ipasavyo vyanzo vya maji, tofauti na mabwawa kama ya Kidatu na Mtera.

Nadhani ukichokonoa zaidi, utagundua kwamba orodha ya vitu kama hivyo ambavyo vinaangamiza makampuni, wananchi ama taifa kwa ujumla lakini kundi dogo la wabinafsi wakifaidi ni ndefu.

Katika bunge la Bajeti lililokwisha mwezi uliopita, Mbunge wa Mkanyageni kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Habib Mnyaa, aliongeza orodha ya kitu kingine ambacho kinaliumiza sana taifa, kutokana na kuhujumiwa na wachache kwa faida zao. Kitu hiki ni reli ya kati.

Mbunge huyo alisema bungeni na nadhani matamshi yake yako kwenye Hansard na sijasikia mahala yalikopingwa kwamba kuna wakubwa wana malori lukuki na hivyo wamekalia kuhujumu Shirika letu la Reli kwa sababu likitengemaa barabara, basi biashara yao ya kusafirisha vitu kwa malori nayo imekufa, jambo ambalo hawataki kuona!

Sikutaka niamini sana maneno hayo, lakini juzi nilikuwa ninaongea na madereva fulani wa malori wakaniambia kwamba nchi hii ina malori mengi sana kuliko mabasi.

“Unajua pale Ubungo (stendi ya mabasi ya kwenda mikoani) kila siku kuna mabasi takriban 400 yanayoingia mle kwa ajili ya safari za mikoani. Lakini hapa Dar es Salaam pekee kuna mtu mmoja tu ana malori takriban 1000,” aliniambia dereva huyo na kuuacha mdomo wangu wazi.

Kuna wakati niliongea na Balozi wa Marekani hapa nchini, Alfonso Lenhardt, na ambaye pia ni balozi wa Marekani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki mambo kadhaa kuhusu mipango ya nchi hiyo katika kuisaidia jumuiya ambapo balozi huyo aligusia baadhi ya vikwazo alivyoviona kwa maendeleo ya Watanzania na ambavyo vinaweza kushughuliwa haraka na Watanzania wenyewe.

Vikwazo hivyo ni foleni za magari katika jiji la Dar es Salaam na pili ni Tanzania kuendelea kutumia usafiri ghali wa barabara badala ya reli ambao ndio usafiri rahisi duniani kote katika kusafirisha mizigo.

Yaani, wakati nchi hii ina bandari ambayo inaweza kuiingizia nchi faida kubwa kutoka kwenye mataifa yanayotuzunguka ambayo hayakujaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na bandari, imeshindwa kufaidika kiasi ambacho ilipaswa kufaidi kutokana na kukosa reli ya uhakika. Yaani reli inayozungumzwa hapa ni hii ya kati iliyojengwa na wakoloni wa Kijerumani ili iunganishe nchi yetu kiuchumi lakini tumeshindwa kuindeleza kutokana na uzembe, ujinga na hujuma mbalimbali. Tumeshindwa hivyo huku tukijua kwamba hata gharama za kuhudumia reli ikishasimama sawasawa ni ndogo kulinganisha na barabara.

Ni reli hii ambayo inafanya bei za vitu katika baadhi ya mikoa iliyo pembezoni kama vile Mara, Kigoma na Kagera kuwa ghali sana kwa sababu vinasafiri kwa njia ya ghali ya barabara.

Niliwahi kuwa pale mjini Musoma wakati fulani nikashangaa kugundua kwamba kama saruji kutoka Uganda ingelikuwa inaruhusiwa kuingia nchini kirahisi, hakuna ambaye mjini humo agelinunua saruji inayozalishwa Tanzania kwa sababu ni ghali kulinganisha na ya Uganda kutokana na usafiri ghali wa barabara.

Nimemua kuandika haya kutokana na ukweli kwamba, baada ya kelele nyingi, hatimaye mwekezaji kutoka India, Rites, ambaye hakusaidia lolote zaidi ya kuliua zaidi shirika letu la reli kufangasha virago na sasa kuna mkakati wa kulifufua upya.

Ninaandika hapa pia nikikumbuka namna wabunge walivyoikalia kooni Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ifumuliwe na fedha nyingi zielekezwe katika kufufua na kuimarisha miundombinu ya reli. Baadaye serikali ilikubali kuongeza fedha.

Lakini swali langu la msingi ni kama kweli tutalifufua shirika hili la reli huku kuna watu wenye nguvu ya pesa wanaotaka kuhakikisha kwamba halinyanyuki ili waendeleze biashara zao za malori.

Sambamba na hilo, nimekuwa ninajiuliza kama uongozi mpya wa Kitanzania utazingatia baadhi ya mambo yaliyosababisha kudorora kwa shirika hilo, hususan wizi, udokozi na ubadhirifu.

Kama ambavyo ubadhirifu umekuwa chanzo cha kufa kwa Shirika letu la Ndege (ATCL), ndivyo inasemekana wafanyakazi walivyokuwa wakilihujumu shirika la reli hadi kuwa mzigo kwa serikali.

Yapo madai kwamba wakati reli ikiwa bado sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977, udhibiti ulikuwa mzuri na hakukuwa na wizi wa kutisha wa mali za shirika, lakini baada ya shirika hilo kuwa mikononi mwa Watanzania, mkubwa mmoja angeliweza kusafirisha mbao zake binafsi kutoka Tabora hadi Dar es Salaa katika behewa zima na shirika lisipate mapato yoyote.

Ni sawa na madai kwamba ndege ya ATCL ingeliweza kwenda, tuseme Dubai, lakini sehemu kubwa ya mizigo iliyobeba ni ya wafanyakazi na mahawara zao, kiasi kwamba shirika haliingizi chochote.

Kwa mantiki hiyo, wakati Watanzania kupitia wabunge wao wakililia kuona shirika lao la reli linanyanyuka basi ni vyema tukajua namna ya kupambana na maadui hao; wenye malori ama Watanzania watakaokabidhiwa kuliendesha lakini kumbe nia yao ni ‘kulila’ shirika.